Miundombinu ya Afya itunzwe -Dkt, Biteko

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameagiza kuweka Mpango Mkakati wa kuhakikisha uwekezaji wa miundombinu uliofanywa na Serikali katika vituo vya ngazi ya Afya ya Msingi inatunzwa.

Dkt. Biteko ametoa agizo hilo akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kufungua Mkutano wa Kwanza wa Kimataifa wa Afya ya Msingi nchini Tanzania tarehe 25 Machi, 2024 jijini Dodoma ambapo amesema miundombinu bora inawezesha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi kwa urahisi zaidi.

Ametoa wito wa kujadili kwa kina namna bora ya kubuni mbinu zitakazowezesha kuongeza kasi ya kuajiri wataalam wa kada mbalimbali za afya hasa zenye upungufu mkubwa.

Pia, ameagiza kuainishwa kwa mikakati ya utoaji wa elimu ya afya kwa jamii ili wananchi waelimishwe kuhusu njia za kuzuia magonjwa, umuhimu wa chanjo na njia zingine za kudumisha afya bora.

Amesisitiza kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ya huduma za afya ya msingi ili kuweza kufahamu maendeleo ya utekelezaji wa Afua mbalimbali za afya na kutambua maeneo ya kuboresha.

Dkt. Biteko pia ameupongeza Mfumo wa M-mama uliobuniwa na Watanzania .

“Kwa furaha kubwa nasimama mbele yenu siku ya leo nikifurahia kuona maono ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuhakikisha mfumo wa usafiri wa dharura kwa wajawazito, waliojifungua na watoto,” amesema Dkt. Biteko.

Amesema, M-mama inaratibiwa katika hospitali za mikoa kupitia waratibu waliopewa mafunzo kwa kupiga namba 115 ambapo waratibu wa m-mama katika kila mkoa wanaweza kutoa huduma hizo.

“Napenda kuwashukuru wadau wetu wa maendeleo Vodacom Tanzania, Vodafone Foundation, USAID, Benki ya Dunia na wadau watekelezaji wa mfumo wa ‘Touch Health’ na ‘Pathfinder International’ kwa mchango wao katika kushirikiana na Serikali kuleta huduma hii inayohitajika kwa wote,” amesema Dkt. Biteko.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *