Mpango aahidi kuacha kazi

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amesema endapo maji hayatawafikia wananchi kama ilivyokusudiwa na Serikali katika mradi wa Same – Mwanga -Korogwe ifikapo Juni, mwaka huu, ataacha kazi.

Dk Mpango ametoa kauli hiyo leo Alhamisi alipotembelea mradi huo ambao chanzo chake ni Bwawa la Nyumba ya Mungu, ambao upo katika Kata ya Kirya, Wilaya ya Mwanga, Kilimanjaro.

“Amri ya Rais (Samia Suluhu Hassan) ni kwamba maji yatoke Mwanga na Same ifikapo Juni mwaka huu, nataka nirudie tena, mjipange vizuri, wasimamieni makandarasi na wataalamu, bahati nzuri wana uwezo, usiku na mchana maji yatoke. Mradi huu umekuwa kero kwa wananchi wa maeneo haya, ni takribani miaka 19 imepita tangu umeahidiwa na kuanza kutekelezwa 2014,”amesema Dk Mpango.

“Kila mtu atimize wajibu wake, kurudi kwa Rais kwamba maji hayotoki…mimi nitaacha kazi, kama maji hayatoki hapa, mimi nikiacha kazi, hao wengine sijui, Katibu Mkuu na waziri wake mimi sijui, kwa hiyo tuelewane vizuri.”

Amewataka watendaji wa Wizara ya Maji kutimiza wajibu wao ikiwamo kuwasimamia makandarasi na wataalamu wanaotekeleza mradi huo pamoja na kuweka kambi kusudi kazi ifanyike usiku na mchana.

Amesema ametoa maagizo hayo ili wananchi wa wilaya za Mwanga, Same na Korogwe wapate maji kama walivyoahidiwa na Serikali.

Hatahivyo Dk Mpango amesema wananchi wameusubiri mradi huo kwa muda mrefu huku wakiwa na kiu ya kuondokana na changamoto ya maji katika maeneo yao.

Kutokana na kusuasua kwake, Dk Mpango amewaagiza wataalamu kutoka Wizara ya Maji kuweka kambi kwenye eneo hilo la mradi na wahakikishe unatekelezwa na kukamilika kama ilivyopangwa.

Aidha Historia inaonyesha mradi huo wa maji ulitolewa ahadi na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete mwaka 2005 wakati akiomba kura kuingia madarakani kwa kipindi cha kwanza. na Ulianza kutekelezwa mwaka 2014 na unatarajiwa kugharimu Sh262 bilioni hadi kukamilika kwake, na ukitarajiwa kunufaisha wakazi 438,000.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *