Wawili washikiliwa kwa utengenezaji silaha.

Jeshi la Polisi Mkoani Shinyanga limekamata silaha tano na watuhumiwa wawili kwa kosa la kutengeneza na kumiliki silaha kinyume na sheria.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga SACP Janeth Magomi amesema mnamo tarehe 13/03/2024 maeneo ya Kitongoji cha Izagala, Kijiji cha Ntundu, Kata ya Busangi, Tarafa na Wilaya ya Kipolisi Msalala Mkoani humo Jeshi la Polisi lilifanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja akiwa na mtambo wa kutengenezea silaha uitwao Vice.

Kamanda Magomi ameeleza kuwa mtuhumiwa huyo amekamatwa akiwa na Silaha tatu aina ya Gobole, maganda matano ya risasi ya kutengeneza kienyeji, maganda manne ya Shotgun, vipande saba vya chuma na mbao mbili za kutengeneza silaha aina ya gobole.

Pia amesema wamekamata vitu mbalimbali zikiwemo bhangi, vitanda, magodoro , yai la mbuni na mkia wa nyumbu na kwamba watuhumiwa wote wawili mara baada ya upelelezi kukamilika watafikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria.

Akielezea kuhusu Kesi mahakamani, Kamanda Magomi amesema jumla ya kesi 13 zimepata mafanikio ambapo, kesi 02 za kubaka washtakiwa wawili walihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela, kesi 02 za wizi washtakiwa wawili walihukumiwa kifungo kati ya miezi 06 mpaka miaka 07 jela, kesi 01 ya kupatikana na bhangi mshtakiwa alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela, kesi 01 kuvunja nyumba usiku na kuiba washtakiwa 02 walihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela, kesi 06 kuingia kwa jinai washtakiwa 06 walihukumiwa kifungo cha miezi mitatu jela na kesi 01 kutishia kuua kwa maneno mshtakiwa mmoja alihukumiwa kwenda jela miezi 03.

“Vilevile Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kitengo cha Usalama barabarani limefanikiwa kukamata jumla ya makosa 3,315 ambapo makosa ya magari ni 2,615 na makosa ya bajaji na pikipiki ni 700 wahusika waliwajibishwa kwa kulipa faini za papo kwa hapo”,amesema Magomi.

Aidha Jeshi la Polisi Mkoani hapo linatoa wito kwa wananchi kuacha vitendo vya kihalifu na vilivyo kinyume na Sheria na kwamba halitasita kumchukulia hatua mtu yeyote atakayejihusisha na vitendo vya namna hiyo.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *