Sekta ya afya kuvutia mataifa ya nje.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema sekta ya afya imekua kwa kiwango kikubwa ndani ya miaka miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan kiasi cha kuvutia nchi nyingine nyingi za Kusini mwa Jangwa la Sahara kuja kutibiwa nchini ukilinganisha na miaka kadhaa iliyopita.

Waziri ummy amesema hayo katika Hafla inafanyika leo katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam kwa Lengo la kuangazia mafanikio ya Rais Samia Suluhu Hassan kwenye kipindi cha miaka mitatu ya Uongozi wake wa nchi.
Waziri Ummy amesema sekta hiyo kwa sasa imejikita zaidi kwenye tiba za kisasa upande wa vipimo ambapo mashine za mionzi ya Citiscan zimeongezwa kutoka 13 hadi kufikia 45 nchi nzima.

Amesema, upande wa Ultrasound kwa sasa zinapatikana mpaka kwenye zahanati ambapo kabla ya Rais Samia kuingia madarakani kulikua na Ultrasound 476 na sasa zipo 665 kwa ajili ya mama wajawazito.

Amesema kwa Upande wa mashine za moyo kutoka mashine moja mpaka mashine nne kwa sasa.

“Wagonjwa wa mataifa mengine wanakuja kupata huduma ya matibanu hapa nchini ikiwemo nchi za Malawi, Uganda, Kenya, Comoro, Burundi na nyingine nyingi, hii ni hatua kubwa kwetu, ” amesema Ummy.

Aidha, Waziri huyo amesema magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo Shinikizo la damu, Kisukari, Figo ndio yanayoongoza kuwa na wagonjwa wengi kutokana na tabia bwete.

“Nawaomba Watanzania kufanya mazoezi na kupunguza matumizi ya vyakula vya mafuta, Sukari na Chumvi ili kutunza afya zao zaidi, ” amesema Mwalimu.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na viongozi mbalimbali wakati akiwasili katika kilele cha Kurasa 365 za Mama Samia.

Nae Meneja Maendeleo na Biashara wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO), Mhandisi Magoti Mtani amesema katika sekta ya hiyo hali ya upatikanaji umeme kwa sasa inaelekea kuzuri ukilinganisha na kipindi kilichopita cha shirika hilo.

Mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Mhandisi Mtani amesema kuwa Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Nyerere (JNHPP) ujenzi wake umefikia asilimia zaidi ya 93 na pindi likikamilika Megawati 2115 zinategemewa kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa.

Amesema mradi wa Gesi wa Kinyerezi 1 Extension una uwezo wa kuingiza Megawati 180, lakini mwaka huu tayari imeingiza Megawati 160 huku mradi wa Maporomoko ya maji Rusumo unaolisha nchi ya Tanzania, Rwanda na Burundi tayari unalisha Megawati 27 kwenye gridi yetu ya taifa.

Kadhalka amesema reli ya SGR itakua na njia (lots) tatu za kusafirishia umeme wa uhakika muda wote ili kuifanya treni hiyo itoe huduma kwa uhakika.

“Hivyo basi, umeme wake utatoka katika njia ambazo zimeunganishwa kutoka maeneo mbali mbali na hii limeweza kufanyika kwa Lots 3 na ya kwanza ni Msamvu – Ihumwa (Lot 1 ina double circuits ambapo inajumuisha Lot 1 – 2 kwa pamoja na Lot ya 3 ni kutoka Isaka – Mwanza,” amesema Mtani

Ameongeza kuwa kuna uwekezaji mkubwa unafanyika katika kufanya umeme kuwa wa uhakika nchini-
“Serikali imefanya kila liwezekanalo na sisi kama shirika, tunahakikisha fedha tunazopewa zinatumika katika mazingira ambayo ni sahihi na mazuri kuhakikisha hali ya umeme nchini inakuaa nzuri, ” amesema Mtani.

Aidha amesema, mpaka sasa miradi yote ya kimkakati ya umeme inayotekelezwa nchini imetumia jumla ya Sh trilioni 8, katika fedha hizo Sh trilioni 7.2 ni fedha za ndani kwa ufadhili wa Serikali Kuu na kutoka kwa wafadhali wa nje ni Sh trilioni 1.69.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *