Watanzania watakiwa kuuthamini Muungano

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Akizungumza kabla ya kuzindua Nembo na kaulimbiu ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Jijini Dododma.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amewataka Watanzania kuendelea  kuulinda, kuuenzi, kujivunia na kuuthamini Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Majaliwa, ameyabainisha leo jijini Dodoma wakati wa hafla ya uzinduzi wa nembo na kaulimbiu ya miaka 60 ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania.

Amesema Watanzania wana kila sababu ya kujivunia muungano wao kutimiza miaka 60.

“Ni ukweli usiopingika kwamba muungano wetu umeendelea kuwa na tija kubwa na kuchagiza maendeleo ya nchi yetu na wananchi wote kwa ujumla ,Kama ulivyo msemo wa Kiswahili Umoja ni nguvu utengano ni udhaifu, muungano wetu umefanya Tanzania liwe Taifa lenye utulivu, mshikamano, nguvu na mfano kwa mataifa mengi Barani Afrika na duniani kwa ujumla.“amesema Majaliwa.

Aidha amewataka Watanzania kutumia uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu kuchagua viongozi wenye nia njema na muungano na ambao watakuwa msingi imara wa muungano.

“Mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi wa serikali za mitaa lazima tuchague viongozi wenye ni njema na muungano wetu, wawe viongozi ambao ni msingi imara wawe wazalendo na wenye kulinda, kuutetea na kuuenzi mungano wetu”amesema Majaliwa

Aidha, amesema katika maadhimisho ya mika 60 ya muungano mwaka huu yatahusisha shughuli mbalimbali ikiwemo uzinduzi wa miradi mbalimbali utakaofanywa na viongozi wakuu wa serikali wa pande zote za muungano.

Majaliwa amesema kuwa Aprili 14 mwaka huu Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dk.Husein Alli Mwinyi anatarajiwa kuzindua rasmi maadhimishi hayo.

“Mara baada ya tukio hilo miradi mbalimbali itazinduliwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa katika pande zote za muungano”amesema Majaliwa

Ametaja tukio jingine kuwa ni maombi ya kitaifa kwaajili ya kuombea muungano ambayo yatafanyika Aprili 22 kitaifa jiji Dodoma yakiongozwa na Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango.

Pia amezitaka  taasisi zinazotoa elimu, ziendelee kufundisha kuhusu muungano kuanzia elimu ya awali ili watoto na vijana wafahamu, wawe walinzi na vinara katika kuuendeleza.

Hata hivyo Waziri Mkuu  ametoa wito kwa wananchi wote wa pande mbili za muungano kujitokeza kwa wingi ili kushuhudia kilele cha sherehe za Muungano  katika Uwanja wa Uhuru, Jijini Dar es Salaam

“Wananchi wote tumieni maadhimisho haya kutafakari tumetoka wapi, tuko wapi na tunaelekea wapi tangu muungano uliopoasisiwa mwaka 1964. Kaulimbiu ya maadhimisho haya ituongoze katika tafakuri hiyo ili kwa pamoja tuendelee kuulinda na kuutetea muungano wetu.“amesema

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo amesema Watanzania wana kila sababu ya kuuenzi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hivyo amewataka Watanzania kutembea kifua mbele kujivunia Muungano huo adhimu ambao umeleta faida lukuki zikiwemo uhusiano mzuri baina ya wananchi wa pande zote mbili katika Nyanja mbalimbali.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *